TATOA Yaipongeza TRA Kwa Kuondoa VAT Kwa Wamiliki wa Malori Machache
Dar es Salaam, Agosti 07, 2026 — Chama cha Wamiliki wa Malori Nchini Tanzania (TATOA) kimeipongeza Serikali, kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kwa uamuzi wa kuondoa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa wamiliki wa malori machache wanaokodiwa na wenye malori mengi — hatua inayotarajiwa kuinua zaidi sekta ya usafirishaji nchini.
Akizungumza wakati wa kikao cha pamoja kati ya viongozi wa TATOA na Menejimenti ya TRA, kilichofanyika ofisini kwa TRA jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa TATOA Bw. Elius Lukumay alisema uamuzi huo, uliofanywa chini ya uongozi wa Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Yusuph Juma Mwenda, unafungua fursa mpya kwa biashara za usafirishaji za ndani na nje ya nchi.
Kwa muda mrefu, wamiliki wa malori machache wamekuwa wakiomba wapatiwe msamaha wa VAT kama ilivyo kwa wenzao wenye malori mengi. Lukumay alisema tamko hili ni habari njema itakayopanua wigo wa kodi, kwa kuwa sekta ya usafirishaji ni kiungo muhimu kinachounganisha sekta nyingine za kiuchumi nchini.
“Tunaomba Kamishna Mkuu utufikishie shukrani zetu kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa hatua hii kubwa itakayoleta mapinduzi kwenye sekta ya usafirishaji na kuongeza ajira nchini,” alisema Lukumay.
Naye Kamishna Mkuu wa TRA, Bw. Yusuph Juma Mwenda, alisema uamuzi huo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuendelea kuiwezesha sekta ya usafirishaji, ambayo ina mchango mkubwa kwa biashara nyingine za ndani na nje ya nchi.
Alisisitiza kuwa TRA ipo kwa ajili ya kuwezesha biashara na kuondoa vikwazo vinavyokwamisha ustawi wa wafanyabiashara, huku ikiendelea kutatua changamoto za kikodi na zisizo za kikodi zinazowakabili. Lengo, alisema, ni kuwawezesha wafanyabiashara kupata faida zaidi na hatimaye kuchangia zaidi katika ulipaji kodi.
